Legal Questions

Questions & Answers

Find answers to common legal questions and learn more about your rights

1

Je, mtu mwenye ulemavu na ambaye ana ndugu zake ambao hawataki kwa makusudi kumpa msaada wa kijamii inavyowezekana anaweza kufanya nini ili apate haki yake ya kupewa msaada wa kijamii kutoka kwa hao ndugu zake?

+

Anaweza kwenda mahakamani (yeye mwenyewe au kwa kutumia mwakilishi) na kuiomba mahakama itoe amri kwa ndugu hao kumlipa kiasi cha fedha kwa kila mwezi (kifungu namba 17 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
2

Ni athari gani zitajitokeza kama bidhaa mbalimbali ambazo ni mahitaji maalum kwa watu wenye ulemavu zitakuwa zinauzwa kwa bei kubwa ambazo katika hali ya kawaida haziko ndani ya uwezo wa maisha ya watanzania walio wengi?

+

Athari zitakazojitokeza kama bidhaa zitumiwazo na watu wenye ulemavu zitakuwa zinauzwa kwa bei ambayo si ya kawaida kwa maisha ya watanzania walio wengi ni pamoja na idadi kubwa ya walemavu nchini kukosa huduma hizo kabisa na pia kupelekea kukosa haki zao zingine za msingi kama vile haki ya kupata elimu kwani mtu mwenye ulemavu wa viungo hatakwenda shuleni bila nyenzo za kujimudu kama vile baiskeli za watu wenye ulemavu wa aina hiyo, kukosa haki ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa na kadhalika.

Sheria Kiganjani
Learn More
3

Je, mtu mwenye ugonjwa wa UKIMWI ni mtu mwenye ulemavu kwa mujibu wa tafsiri ya sheria?

+

Hapana, mgonjwa wa UKIMWI si mtu mwenye ulemavu kisheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
4

Je, mwanamke mjamzito ni mfano mojawapo wa watu wenye ulemavu?

+

Hapana, mwanamke mjamzito si mtu mwenye ulemavu kwani kuwa na ujauzito si tatizo, si hali ya kudumu na wala ujauzito haumfanyi mwanamke kushindwa kushiriki katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii.

Sheria Kiganjani
Learn More
5

Je, ni lazima kwa mtu mwenye ulemavu kuendelea kuwa tegemezi kwa ndugu zake?

+

Hapana, si lazima kwa mtu mwenye ulemavu kuwa tegemezi kwa ndugu zake. Ana haki ya kujitegemea ilimradi ana uwezo wa kufanya hivyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
6

Tafiti zinaonesha kuwa watu wenye ulemavu wanachukizwa na baadhi ya maneno ya lugha ya Kiswahili yanayotumika kuwarejelea. Maneno hayo ni kama vile kilema, kipofu, zezeta (taahira) na kiwete. Ni kwanini watu wenye ulemavu wanachukizwa na maneno hayo na unapendekeza warejelewe kwa kutumia maneno gani badala ya hayo yaliyotajwa ili, pamoja na mambo mengine, kulinda haki yao kuheshimiwa katika jamii?

+

Katika hali ya kawaida, maneno hayo yanawakejeli na kutweza utu wao na yanawafanya wajisikie kama wananyanyapaliwa katika jamii. Badala ya maneno hayo maneno kama mlemavu, asiyeona, mwenye ulemavu wa akili na mlemavu wa viungo yatumike kuwarejelea watu wenye ulemavu wa aina hizo.

Sheria Kiganjani
Learn More
7

Je, mfanyakazi mwenye ulemavu wa viungo ana haki ya kupata mshahara au posho sawa na wafanyakazi wengine ambao si walemavu au inategemea busara za mwajiri?

+

Mwajiri hatakiwi kumbagua mfanyakazi mwenye ulemavu katika suala la mshahara au posho. Hivyo, mfanyakazi mwenye ulemavu wowote ana haki ya kupata mshahara au posho sambamba na wafanyakazi wenzake.

Sheria Kiganjani
Learn More
8

Je, mtu mwenye ulemavu ana wajibu wa kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya taifa?

+

Ndiyo, anawajibu kama watu wengine kufanya kazi na kuleta maendeleo katika taifa

Sheria Kiganjani
Learn More
9

Je, ni wajibu kisheria kwa Halmashauri za wilaya kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika mipango na mikakati ya Serikali?

+

Ndiyo, Halmashauri za wilaya zina wajibu wa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika mipango na mikakati ya Serikali.

Sheria Kiganjani
Learn More
10

Je, chuo chochote kikianzishwa kikawa na miundombinu yote ambayo si rafiki kwa matumizi ya watu wenye ulemavu kinatafsiriwa kisheria kuwa kimefanya ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu?

+

Ndiyo, huo unakuwa ni ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu chini ya kifungu namba 28 (2) (f) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010.

Sheria Kiganjani
Learn More
11

Je, Mahakama ina uwezo wa kutoa amri kwa mtu yeyote anayemtunza mtoto mwenye ulemavu kumpa mtoto huyo mahitaji yake maalum wakati mtu huyo si baba wala mama yake?

+

Ndiyo, mahakama inaweza kutoa amri kwa mtu yeyote anayemtunza mtoto mwenye ulemavu kumtimizia mahitaji yake maalum chini ya kifungu namba 21 (3) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010.

Sheria Kiganjani
Learn More
12

Je, ni lazima kisheria mtu aombe na kupata idhini ya Serikali kabla ya kuanzisha na kuendesha makazi ya watu wenye ulemavu?

+

Ndiyo, mtu yeyote anayetaka kuanzisha makazi ya watu wenye ulemavu anahitaji idhini ya Serikali kupitia kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii.

Sheria Kiganjani
Learn More
13

Je, ni lazima kisheria kwa kiongozi mkuu wa taasisi ya umma inayotoa huduma yoyote kuhakikisha huduma hiyo inayotolewa na taasisi hiyo inapatikana pia kwa watu wenye ulemavu?

+

Ndiyo, ni lazima kufanya hivyo kwa mujibu wa kifungu namba 37 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010.

Sheria Kiganjani
Learn More
14

Unaelewa nini juu ya “shule jumuishi”?

+

Ni shule ambayo vikwazo vyote vinavyoweza kuwazuia wanafunzi wenye ulemavu kusoma na kutimiza haki yao ya kielimu vimeondolewa. Yaani, shule ambayo mwanafunzi mwenye ulemavu anaweza kusoma bila vikwazo vyovyote kwa mfano vya kimazingira kama vile majengo kufikika n.k.

Sheria Kiganjani
Learn More
15

Je, nani mwenye wajibu kisheria kuhakikisha mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu yanapatikana kirahisi kwa bei ambayo ni ya chini iwezekanavyo na ambayo katika hali ya kawaida iko ndani ya uwezo wa maisha ya watanzania?

+

Serikali ndiyo yenye wajibu huo.

Sheria Kiganjani
Learn More
16

Upi ni umuhimu wa shule jumuishi?

+

Shule jumuishi ni muhimu sana kwani huwawezesha watu wenye ulemavu kupata haki yao ya kielimu bila vikwazo vyovyote vinavyowafanya wasitimize haki yao ipasavyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
17

Tofautisha kati ya “ubaguzi chanya” kwa watu wenye ulemavu na “ubaguzi hasi” dhidi ya watu wenye ulemavu.

+

Ubaguzi chanya kwa watu wenye ulemavu ni sera ambazo huwapendelea watu wenye ulemavu katika upatikanaji wa huduma mbalimbali wakati ubaguzi hasi dhidi ya watu wenye ulemavu ni kitendo cha kumtofautisha mtu mwenye ulemavu na watu wengine katika upatikanaji wa huduma kwa kumfanya mtu mwenye ulemavu asipate haki yake ya msingi kama binadamu kwa kigezo tu cha kuwa na ulemavu huo.

Sheria Kiganjani
Learn More
18

Upi ni umuhimu kisheria wa kuzingatia uwepo na mahitaji ya watu wenye ulemavu katika kutunga sheria za nchi?

+

Umuhimu wa kuzingatia uwepo na mahitaji ya watu wenye ulemavu wakati wa kutunga sheria za nchi ni kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa ipasavyo bila kufanyiwa ubaguzi wowote wenye madhara hasi dhidi yao.

Sheria Kiganjani
Learn More
19

Kwa mujibu wa Sheria, Serikali ina wajibu wa kufanya tafiti kuhusu masuala mbalimbali juu ya watu wenye ulemavu nchini. Je, unadhani utafiti juu ya watu wenye ulemavu una faida gani?

+

Utafiti kuhusu mambo yanayowahusu watu wenye ulemavu una faida kama vile kufahamu idadi kamili ya watu wenye ulemavu katika sehemu husika kama vile wilaya au mkoa, kufahamu aina za ulemavu walio nao, kufahamu kama watu hao wenye ulemavu wanapata mahitaji yao maalum, kufahamu kama watu wenye ulemavu wanapatiwa misaada ya kijamii kutoka kwa ndugu zao, kufahamu sababu mbalimbali zinazosababisha ulemavu kwa kiwango kikubwa pamoja na kufahamu namna ya kuweza kukabiliana na mambo mbalimbali yasabababishayo ulemavu kwa watu walio wengi katika jamii.

Sheria Kiganjani
Learn More
20

Wizara gani inashughulika na watu wenye ulemavu nchini?

+

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

Sheria Kiganjani
Learn More
21

Je, nani ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Serikali ya Mtaa juu ya uvunjwaji wa haki ya mtoto mwenye ulemavu?

+

: Kwa mujibu wa kifungu namba 21 (1) cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010, mtu yeyote katika jamii anaweza kutoa taarifa juu ya uvunjwaji wa haki ya mtoto mwenye ulemavu unaofanywa na mzazi, mlezi au mtu yeyote anayemlea mtoto huyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
22

: Je, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kuchaguliwa kuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

+

: Ndiyo, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kushiriki katika mambo yote ya kisiasa ikiwemo kuchaguliwa kuwa kiongozi yeyote kama vile Mbunge n.k.

Sheria Kiganjani
Learn More
23

Mtu yeyote anaruhusiwa kisheria kuanzisha na kumiliki shule maalum ya watu wenye ulemavu. Je, mtu huyo anayeanzisha na kumiliki shule maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu anakuwa na wajibu gani wa jumla kisheria?

+

Anakuwa na wajibu wa jumla kuhakikisha shule hiyo ina vifaa vya kutosha vinavyohitajika kwa matumizi ya wanafunzi hao wenye ulemavu (kif. 29 (2) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
24

Je, Baraza la Taifa la Ushauri wa Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu linaundwa na watu gani?

+

Baraza hili huundwa na; i. Mwenyekiti wa Baraza ambaye huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ii. Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali iii. Mwakilishi kutoka wizara zinashoshughulikia mambo ya afya, serikali za mitaa, utumishi wa umma, maendeleo ya jamii, kazi na elimu iv. Mwakilishi kutoka Chama cha Waajiri Tanzania v. Mwakilishi kutoka Shirika la Watu Wenye Ulemavu vi. Mjumbe kutoka Tume ya Haki na Utawala Bora, na vii. Wajumbe wengine watano wanaoteuliwa na Waziri anayehusika na watu wenye ulemavu (Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu).

Sheria Kiganjani
Learn More
25

Kamishna wa Ustawi wa Jamii ana wajibu kisheria kuanzisha na kutunza daftari la orodha ya watu wenye ulemavu. Upi ni umuhimu wa kuwa na daftari hili la orodha ya watu wenye ulemavu?

+

Daftari hili la orodha ya watu wenye ulemavu husaidia kufahamu idadi ya watu wenye ulemavu katika eneo husika na ni ulemavu wa aina gani. Husaidia pia kujua mahitaji maalum kwa kila mtu mwenye ulemavu na kuweza kuchukua hatua zinazostahili katika wakati unaostahili na kwa kutumia njia zinazostahili.

Sheria Kiganjani
Learn More
26

Je, nini kinatakiwa kufanyika kama kituo cha kupigia kura kiko mahali ambapo hapawezi kufikika kwa mtu mwenye ulemavu wa viungo?

+

Eneo lingine lenye uwezekano wa kufikika kwa mtu mwenye ulemavu huo linatakiwa kutafutwa na kutangazwa hivyo ili mtu huyo mwenye ulemavu aweze kutimiza haki yake (Kifungu namba 51 (4) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
27

“Lugha ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana na ambao hutumiwa na watu ili kuwasiliana” (TUKI, 2000). Ni kwa namna gani fasili au ainisho hiyo inawabagua watu wenye ulemavu?

+

Fasili hii inaibagua lugha ya alama ambayo ni njia ya mawasiliano kwa baadhi ya watu wenye ulemavu kama vile wasiosikia (viziwi), bubu na bubuviziwi.

Sheria Kiganjani
Learn More
28

Je, mkurugenzi au meneja wa hospitali ya Umma au isiyo ya umma (yaani hospitali inayomilikiwa na mtu binafsi) ana haki ya kuamua asiwape huduma yoyote ya kiafya watu wenye ulemavu kwa kigezo tu cha ulemavu wao?

+

Hapana, hawezi kuwanyima watu wenye ulemavu haki yao ya kupatiwa huduma ya kiafya kwa kigezo cha ulemavu wao (kifungu namba 26 (2) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
29

Je, kwa mujibu wa maana ya mtu mwenye ulemavu kisheria, mtu anayekula na kuandika kwa kutumia mkono wa kushoto tu ilihali ana mikono yote ni mtu mwenye ulemavu?

+

Hapana, kutumia mkono wa kushoto wakati wa kula na kuandika si ulemavu kisheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
30

Mtu mwenye ulemavu ambaye jina lake lilikwishaorodheshwa kwenye orodha ya watu wenye ulemavu na Kamishna wa Ustawi wa Jamii; Je, ana haki ya kutoa jina lake kwenye orodha hiyo ilihali bado ana ulemavu huo?

+

Hapana, kwa mujibu wa kifungu namba 24 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010, mtu mwenye ulemavu hawezi kutoa jina lake kwenye orodha ya watu wenye ulemavu wakati bado ana ulemavu huo.

Sheria Kiganjani
Learn More
31

Je, ni lazima Serikali kumchagulia mtu mwenye ulemavu eneo la kuishi?

+

Hapana, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kuchagua yeye mwenyewe eneo lake la kuishi ilimradi afuate sheria husika (kifungu cha 15 (3) (a) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
32

Je, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuamua kutomsajili mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino) kama mpiga kura kwa kigezo tu cha kuwa na ulemavu huo tajwa?

+

Hapana, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kusajiliwa kupiga kura kama watu wengine. Hivyo, kigezo tu cha kuwa mlemavu wa ngozi hakitoshi kuwa sababu ya kutokusajiliwa kama mpiga kura.

Sheria Kiganjani
Learn More
33

Je, shule maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu zinatakiwa kisheria kuendelea kuwa hivyo hivyo kwa ajili ya watu wenye ulemavu pekee kwa miaka yote?

+

Hapana, shule maalum zinazoanzishwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu zinatakiwa kuwa hivyo kwa kipindi cha mpito tu na baadaye kubadilika na kuwa shule jumuishi (kwa mujibu wa kif. 29 (3) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
34

Je, ni halali kwa vyombo vya habari kama vile redio na televisheni kuendesha vipindi ambavyo vinahimiza mitazamo na taswira hasi dhidi ya walemavu?

+

Hapana, si halali kabisa kwa vyombo vya habari kuendesha vipindi vinavyohimiza taswira hasi dhidi ya watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
35

Je, uteuzi wa baadhi ya watu wenye ulemavu katika ngazi mbalimbali za maamuzi ndani ya Serikali kuwawakilisha walemavu wenzao ni kinyume na sheria?

+

Hapana, si kinyume na sheria kwani wana haki ya kushirikishwa kwenye mambo yote ya kisiasa na kuteuliwa kwenye ngazi zote za Serikali (kif. 51 (5) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010) na pia unakuwa ni ubaguzi chanya kwa ajili ya ustawi wa watu wenye ulemavu kwa ujumla.

Sheria Kiganjani
Learn More
36

Ni kosa la jinai kumsababishia mtu ulemavu kwa makusudi (vifungu namba 231 na 232 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania). Je, idhini ya aliyesababishiwa ulemavu huo inaweza kumtoa mtu aliyesababisha ulemavu huo katika jukumu la jinai?

+

Hapana. Idhini ya aliyesababishiwa ulemavu haimtoi mtu aliyesababisha ulemavu huo kwenye jukumu la jinai. Hivyo, hata kama mtu akikubali mwenyewe kusababishiwa ulemavu, hairuhusiwi kwa mtu yeyote kumsababishia mwenzake ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
37

Ndiyo, mtu mwenye ulemavu ana wajibu wa kuwaheshimu watu wengine.

+

Hapana. Mtu mwenye ulemavu ana wajibu wa kutii sheria kama watu wengine.

Sheria Kiganjani
Learn More
38

Taja sababu tano ambazo mara nyingi husababisha ulemavu kwa watu wa Tanzania.

+

i. Ajali mbalimbali hasa za barabarani na sehemu za kazi ii. Ukosefu wa chanjo kwa watoto dhidi ya magonjwa yanayoleta ulemavu iii. Magonjwa kwa wanawake wajawazito au matatizo wakati wa kujifungua ambayo husababisha ulemavu kwa mama mwenyewe au mtoto aliyezaliwa iv. Urithi kutoka kwa wazazi v. Lishe duni na umaskini

Sheria Kiganjani
Learn More
39

Je, unadhani zipi ni changamoto ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakutana nazo katika suala zima la utekelezaji wa wajibu wake wa kisheria wa kuhakikisha inakuza na kuinua vipaji vya watu wenye ulemavu?

+

i. Baadhi ya watu bado wana imani potofu dhidi ya watu wenye ulemavu kwani huwaficha na hivyo Serikali kushindwa kuwapata au kuwaona. ii. Baadhi ya familia zinazowatunza watu wenye ulemavu haziwaruhusu watu hao wenye ulemavu kuonesha vipaji vyao kama vile kuwaruhusu kwenda kushiriki michezo ili wenye vipaji hivyo waonekane na kadhalika. iii. Badhi ya watu wenye ulemavu wenyewe hawapendi kuonesha vipaji vyao, hivyo inakuwa vigumu kwa Serikali kujua nani ana kipaji gani.

Sheria Kiganjani
Learn More
40

Je, unadhani ni changamoto gani hujitokeza wakati wa utekelezaji wa mahitaji ya watu wenye ulemavu?

+

i. Changamoto ya ukosefu wa elimu ya kutosha kwa jamii ii. Changamoto ya kiuchumi kuwanunulia watu wenye ulemavu nyenzo za kujimudu kama vile baiskeli za watu wenye ulemavu wa viungo n.k. iii. Changamoto ya mawasiliano hususani kwa watu wenye ulemavu ambao hawajapelekwa kwenye mafunzo ya lugha ya alama au nukta nundu n.k.

Sheria Kiganjani
Learn More
41

Unashauri nini kifanyike ili kuondoa misimamo na imani potofu za jamii dhidi ya watu wenye ulemavu?

+

i. Elimu iendelee kutolewa kwa jamii ii. Adhabu kali zitolewe kwa watu wanaofanya vitendo viovu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Sheria Kiganjani
Learn More
42

Taja taasisi tano zenye wajibu wa kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu.

+

i. Familia ii. Jamii iii. Idara ya Ustawi wa Jamii iv. Baraza la Taifa la Ushauri wa Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu v. Mahakama

Sheria Kiganjani
Learn More
43

Kwa mujibu wa sheria, majengo yote yanayotoa huduma kwa umma yanatakiwa kuwa na dawati linaloshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu au mtaalamu yeyote kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Je, ni kwanini busara za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliona kuna umuhimu wa jambo hili?

+

i. Ili iwe rahisi kwa watu wenye ulemavu kupata huduma na pale inapohitajika, waweze kupata huduma zinazoendana na mahitaji yao. ii. Inakuwa ni rahisi kueleza na kueleweka kwa shida au mahitaji yao kwa wataalamu wa mambo yahusuyo watu wenye ulemavu kuliko kuwaelezea watu wasio waelewa sana wa mambo hayo. iii. Inawafanya watu wenye ulemavu kuelezea mahitaji au shida zao kwa uhuru.

Sheria Kiganjani
Learn More
44

Kisheria, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kuajiriwa katika sekta ya umma au sekta binafsi. Je, ni kwa mazingira gani mtu mwenye ulemavu hawezi kupata haki hii?

+

i. Kama hakuna nafasi iliyoko wazi ii. Kama mtu huyo mwenye ulemavu hana sifa zinazohitajika iii. Kama mtu huyo mwenye ulemavu hajafanya maombi ya kazi husika au hajaonesha uhitaji wa kazi hiyo. iv. Kama kutokana na asili ya kazi hiyo au hali ya mazingira ya ufanyaji wa kazi hiyo, ni ngumu au haiwezekani kufanywa na mtu mwenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
45

Kuna Baraza la Taifa la Ushauri wa Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ambalo linaanzishwa chini ya kifungu namba 8 (1) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010. Je, nini majukumu ya Baraza hili?

+

i. Majukumu ya Baraza hili ni pamoja na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mambo yote yanayowahusu watu wenye ulemavu, kuyawasilisha mahitaji na matatizo mbalimbali yanayowasibu watu wenye ulemavu kwa Serikali. ii. Kuishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi juu ya namna bora ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kutimiza haki yao ya kushiriki katika uchaguzi. iii. Kushauri njia zinazoweza kufanyika kupunguza ongezeko la watu wenye ulemavu kwa kiwango kinachowezekana na kadhalika.

Sheria Kiganjani
Learn More
46

“Msimamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu ni kizuizi katika maendeleo yao.” Je, ni misimamo gani katika baadhi ya jamii za Tanzania ambayo ni kizuizi katika maendeleo ya watu wenye ulemavu na ambayo iko kinyume na haki za walemavu.

+

i. Msimamo kwamba watu wenye ulemavu wa kuona au kusikia hawawezi kupata elimu au mafunzo ii. Imani za watu kwamba watu wenye wenye ulemavu hawawezi kuajiriwa wakafanya kazi kama wengine iii. Imani za kuwaficha watu wenye ulemavu wakiamini kuwa ni nuksi na laana kwa jamii

Sheria Kiganjani
Learn More
47

Zipi ni faida za nyenzo za kujimudu kwa watu wenye ulemavu?

+

i. Nyenzo za kujimudu huwasaidia watu wenye ulemavu kumudu mazingira ii. Nyenzo za kujimudu huwasaidia watu wenye ulemavu kufanya kazi na kujipatia kipato iii. Nyenzo za kujimudu huwasaidia watu wenye ulemavu kushiriki vema katika shughuli za kiutamaduni kama vile michezo na kadhalika, kwani walemavu wa viungo hutumia baiskeli zao kufanya mashindano ya mbio na michezo ya aina nyingine.

Sheria Kiganjani
Learn More
48

Je, taasisi zinazohusika na suala la afya kama vile hospitali, vituo vya afya na zahanati zina wajibu gani katika kulinda haki ya watu wenye ulemavu kupata huduma bora za kiafya?

+

i. Taasisi za afya zina wajibu wa kutoa huduma za kiwango sawa kwa watu wote bila ubaguzi kwa misingi ya ulemavu wowote. ii. Taasisi za afya zina wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohitajika kipekee kwa watu wenye ulemavu katika maeneo yao. iii. Kuwapatia elimu na ushauri watu wenye ulemavu na kuheshimu utu wao kadri inavyowezekana.

Sheria Kiganjani
Learn More
49

Unadhani upi ni umuhimu wa watu wenye ulemavu kuwa na vyama au asasi zao hapa nchini Tanzania?

+

i. Vyama vya watu wenye ulemavu husaidia kurahisisha uwasilishaji wa changamoto zao katika sehemu husika ii. Vyama vya watu wenye ulemavu huwakutanisha pamoja watu wenye ulemavu na kubadilishana mawazo mbalimbali iii. Vyama vya watu wenye ulemavu hufanya watu wenye ulemavu waonekane na jamii kuweza kuchukua hatua mbalimbali zinazostahili iv. Vyama vya watu wenye ulemavu pia husaidia katika suala zima la utoaji wa elimu kwa jamii nzima juu ya namna bora ya kutekeleza mahitaji ya watu wenye ulemavu hapa nchini. v. Kupigania haki za watu wenye ulemavu

Sheria Kiganjani
Learn More
50

Kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010, kila kijiji au mtaa ki/unatakiwa kuwa na kamati inayohusika na watu wenye ulemavu. Je,nini umuhimu wa kamati hizi, ilihali zipo kamati za wilaya na mikoa?

+

Ili iwepo kamati ya kushughulikia haki na stahiki za watu wenye ulemavu ambayo iko karibu moja kwa moja na jamii katika vijiji au mitaa. Pia ni rahisi zaidi kwa Serikali ya kijiji au mtaa kushughulikia mambo yanayowahusu watu wenye ulemavu katika vijiji au mitaa kwasababu wako karibu nao.

Sheria Kiganjani
Learn More
51

Kwa mujibu wa kifungu namba 31 (4) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010, kila mwajiri ana wajibu wa kuwasilisha taarifa kila mwaka kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii juu ya ajira za watu wenye ulemavu katika taasisi husika. Je, ni kwanini Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliamua kutunga kifungu hiki kidogo cha sheria?

+

Ili kuwataka waajiri wawajibike kuwaajiri watu wenye ulemavu katika taasisi zao na kutowafukuza au kuwasimamisha kazi bila sababu za msingi kwani bila kuwataka kuwasilisha taarifa kila mwaka waajiri wanaweza kutotimiza wajibu wa kutoa ajira kwa watu wenye ulemavu. Pia kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki yao ya kuajiriwa kwenye taasisi za umma na binafsi bila kubaguliwa ilimradi wana sifa za msingi kupata ajira hizo.

Sheria Kiganjani
Learn More
52

Je, hali ya utulivu wa maisha ya mtu mwenye ulemavu katika jamii kutokana na kutimizwa kwa mahitaji yake muhimu inaitwaje?

+

Inaitwa “Utengemao”.

Sheria Kiganjani
Learn More
53

Kwa mujibu wa Ibara ya 18(2) ya Katiba ya Tanzania, ni haki ya kila raia kupewa taarifa kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani. Nini umuhimu wa kifungu hichi?

+

Kifungu hiki cha sheria kinatambua haki ya kila mtu kupata elimu na habari zinazohusu mambo ya kitaifa ambazo kwa namna moja au nyingine, hugusa maisha ya watu wote katika taifa. Kwa mantiki hiyo, kifungu hiki kinalinda haki ya watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) kupata elimu pamoja na habari mbalimbali zinazolihusu taifa kwa ujumla kwani bila kutumia lugha ya alama, kundi hili halitaweza kupata elimu au habari hizo nyeti.

Sheria Kiganjani
Learn More
54

Kwa mujibu wa kifungu namba 137 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania (kama ilivyofanyiwa marejeleo mwaka 2022), ni kosa la jinai kwa mwanaume yeyote kufanya au kujaribu kufanya ngono isiyo halali na mwanamke ambaye anamfahamu kuwa ni punguani au juha (mwenye ulemavu wa akili) hata kama ni kwa mazingira ambayo si ya kubaka. Je, kifungu hiki cha sheria kinalindaje haki za wanawake au wasichana wenye ulemavu wa akili?

+

Kifungu hiki cha sheria kinatambua kuwa baadhi ya wanaume huweza kutumia nafasi ya ulemavu wa akili kwa mwanamke na kufanya naye tendo la ngono lisilo halali kwa kisingizio cha kwamba mwanamke huyo aliridhia mwenyewe na hakuna nguvu iliyotumika. Hali hii yaweza kuwafanya wanawake wenye ulemavu wa akili kupata magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa. Hivyo, kifungu hiki kinalinda haki ya wanawake wenye ulemavu wa akili kutofanyiwa vitendo vya ngono bila ridhaa iliyotolewa wakiwa na akili timamu

Sheria Kiganjani
Learn More
55

Je, taasisi ya elimu kama vile chuo kina wajibu gani wa jumla kisheria kwa wanafunzi wote wenye ulemavu kwa ujumla?

+

Kutowabagua kwa aina yoyote wanafunzi wenye ulemavu au kuonesha ishara yoyote inayoleta ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
56

Serikali ina wajibu kisheria wa kuhamasisha uteuzi wa watu wenye ulemavu katika nyadhifa mbalimbali kwenye ngazi mbalimbali za Serikali. Je, umuhimu wa hili ni nini?

+

Kuwawezesha na kuwapa nafasi watu wenye ulemavu kushiriki ipasavyo katika uongozi na mambo ya kisiasa kwa ujumla.

Sheria Kiganjani
Learn More
57

Nini maana ya makazi ya watu wenye ulemavu?

+

Makazi ya watu wenye ulemavu ni maeneo au majengo ya umma yaliyoanzishwa kwa dhumuni la kutoa matunzo na mahitaji ya msingi kwa watu wenye ulemavu kwa ajili ya ustawi wao.

Sheria Kiganjani
Learn More
58

Upi ni umuhimu wa kuwa na mchangamano katika jamii?

+

Mchangamano katika jamii ni muhimu kwani huondoa unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu, huwafanya watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za kuwaletea maendeleo kiuchumi na kijamii na kupata haki zao zote sambamba na watu wengine.

Sheria Kiganjani
Learn More
59

Unaelewaje kuhusu mchangamano katika jamii?

+

Mchangamano ni kiwango cha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maisha na kazi za jamii. Dhana hii hujumuisha taratibu za utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu kwa kutumia taasisi na vyombo vile vile vinavyotumiwa na watu wasio na ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
60

Nini maana ya mtu mwenye ulemavu?

+

Mtu mwenye ulemavu ni mtu mwenye matatizo ya muda mrefu au ya kudumu kimwili, kiakili au kihisia ambayo humfanya ashindwe na kuzuia ushiriki wake kikamilifu sawa na watu wengine katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii.

Sheria Kiganjani
Learn More
61

Je, mtu mwenye ulemavu wa kuona (kipofu) ana haki ya kupata mafunzo ya ufundi katika chuo chochote kilichosajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE)?

+

Ndio, kwasababu watu wenye ulemavu wa aina yoyote wana haki ya kupata elimu au mafunzo kama ilivyo kwa raia wengine.

Sheria Kiganjani
Learn More
62

Je, mtu mzima mwenye umri kuanzia miaka kumi na nane (18) anayekuwa mlemavu baada ya kugongwa na gari barabarani kwa uzembe wake mwenyewe ana haki ya kupata msaada kutoka kwa ndugu zake?

+

Ndiyo, ana haki hiyo ilimradi tu ni mlemavu. Namna mtu alivyopata ulemavu haimtofautishi na walemavu wengine wa aina yake.

Sheria Kiganjani
Learn More
63

Je, mtu asiyeona wala kusikia ana haki ya kupata matangazo ya kazi kwa kutumia nukta nundu kama njia yake ya mawasiliano?

+

Ndiyo, ana haki yakupata taarifa hizo.

Sheria Kiganjani
Learn More
64

Je, mashirika au asasi zisizo za kiserikali zinaruhusiwa kisheria kupigania au kufanya harakati za haki za watu wenye ulemavu Tanzania?

+

Ndiyo, asasi zisizo za kiserikali zinaruhusiwa kufanya harakati za haki za watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
65

Je, kuna umuhimu wowote wa kuwa na asasi au mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na uanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu?

+

Ndiyo, asasi zisizo za kiserikali zinazofanya uanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu zina umuhimu kwani husaidia kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu na jamii kuondokana na baadhi ya mitazamo na imani hasi dhidi ya watu wenye ulemavu. Asasi hizi pia husaidia kuikumbusha Serikali kutimiza wajibu wake katika suala zima la kulinda haki za watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
66

Ni haki ya kila mtu kushiriki katika shughuli za kiutamaduni. Je, mtu mwenye ulemavu wa viungo ana haki ya kucheza ngoma?

+

Ndiyo, kuwa mlemavu wa aina yoyote hakuondoi haki yake.

Sheria Kiganjani
Learn More
67

Je, sheria zote zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinatakiwa kuzingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu?

+

Ndiyo, kwa mujibu wa kifungu namba 5 (1) (b) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010, sheria zote zinazotungwa zinatakiwa kuzingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu nchini.

Sheria Kiganjani
Learn More
68

Je, lugha ya alama inayotumiwa na baadhi ya walemavu kama vile wasioona, (viziwi) na bubu ni njia rasmi ya mawasiliano kwa mujibu wa sheria?

+

Ndiyo, lugha ya alama ni njia rasmi ya mawasiliano kwa mujibu wa kifungu namba 53 (4) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010.

Sheria Kiganjani
Learn More
69

Je, maofisa katika tasnia za utoaji haki kama vile polisi na wafanyakazi wa magereza wana wajibu wa kuheshimu haki za watu wenye ulemavu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kisheria?

+

Ndiyo, maofisa wa tasnia za utoaji haki wana wajibu wa kuheshimu haki za watu wenye ulemavu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Sheria Kiganjani
Learn More
70

Kila mtu ana haki ya kumiliki mali. Je, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kumiliki ardhi?

+

Ndiyo, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kumiliki ardhi kama watu wengine.

Sheria Kiganjani
Learn More
71

Je, mtu mwenye ulemavu ana wajibu wa kuwaheshimu watu wengine?

+

Ndiyo, mtu mwenye ulemavu ana wajibu wa kuwaheshimu watu wengine. 

Sheria Kiganjani
Learn More
72

Je, mwajiri yeyote aliyewaajiri watu wenye ulemavu ana wajibu kisheria wa kujitahidi awezavyo kulinda na kudumisha ajira za watu hao wenye ulemavu?

+

Ndiyo, mwajiri yeyote aliyemwajiri mtu mwenye ulemavu ana wajibu kuhakikisha analinda na kudumisha ajira ya mtu huyo mwenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
73

Je, ni kosa kisheria kwa mzazi wa mtoto mwenye ulemavu kumficha mtoto huyo na kukataa kumpeleka shuleni kwa sababu yoyote ile?

+

Ndiyo, ni kosa la jinai kumficha mtoto mwenye ulemavu na kutompeleka shuleni kwa sababu yoyote ile.

Sheria Kiganjani
Learn More
74

Je, ni kosa la jinai kumzuia mtu mwenye ulemavu kuingia katika ofisi yoyote ya umma?

+

Ndiyo, ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu namba 50 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010.

Sheria Kiganjani
Learn More
75

Je, ni wajibu wa Serikali kisheria kuhakikisha uwepo wa mafunzo ya wataalamu wenye weledi wa kufanyia kazi mambo yanayowahusu watu wenye ulemavu?

+

Ndiyo, ni wajibu wa Serikali (hususani Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum) kuhakikisha uwepo wa wataalamu wenye weledi wa kushughulikia mambo yawahusuyo watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
76

Je, nukta nundu ambazo hutumiwa na watu wasioona (vipofu) ni njia rasmi na halali ya mawasiliano kwa mujibu wa sheria?

+

Ndiyo, nukta nundu ni njia halali ya mawasiliano kwa mujibu wa sheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
77

Je, Serikali ina wajibu kisheria kuhakikisha uwezeshaji wa watu wenye ulemavu kukuza vipaji vyao kama vile uimbaji, michezo, utangazaji na kadhalika?

+

Ndiyo, Serikali ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi kuhakikisha ukuzaji wa vipaji mbalimbali vya watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
78

Je, serikali ya kijiji au mtaa ina wajibu wa kulinda haki ya mtu mwenye ulemavu?

+

Ndiyo, Serikali ya kijiji au mtaa ina wajibu huo.

Sheria Kiganjani
Learn More
79

Je, Sheria inamlinda mwajiriwa aliyepata ajali sehemu ya kazi na kupata ulemavu?

+

Ndiyo, sheria inamlinda mfanyakazi yeyote (mwajiriwa) anayepata ulemavu akiwa kazini kwani ana haki ya kurudi na kuendelea na ajira yake (kif. 34 (1) (b) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
80

Je, sheria inatambua vyama na asasi mbalimbali za watu wenye ulemavu hapa nchini?

+

Ndiyo, sheria inatambua vyama na asasi za watu wenye ulemavu (mfano chini ya vifungu namba 57 (3) (c), 5 (4), 9 (i), 11 (e) na (g) na kadhalika vya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More
81

Je, unadhani si sahihi kwa mwalimu mkuu wa shule yoyote kuwazuia wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (albino) kuvaa kofia wakati wa jua kwa sababu tu kwamba wanapaswa kuwa sawa na wanafunzi wenzao?

+

Ndiyo, si sahihi kabisa kwani kofia ni mahitaji maalumu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na ni muhimu kwao kuvaa.

Sheria Kiganjani
Learn More
82

Je, ujenzi wa viwanja vya michezo unatakiwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu?

+

NDIYO, ujenzi wa viwanja vya michezo unatakiwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kuwafanya waweze kumudu mazingira ya michezo kwa urahisi na kutimiza haki yao ya kushiriki katika michezo.

Sheria Kiganjani
Learn More
83

“Ujumuishaji wa watu wenye ulemavu” ni nini?

+

Ni kitendo au mchakato wa watu kwenye jamii kuthamini na kuheshimu tofauti za watu kimwili na kiakili na hivyo kuondoa au kupunguza vikwazo dhidi ya watu wenye ulemavu kuweza kushiriki vema katika shughuli za jamii na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Sheria Kiganjani
Learn More
84

Licha ya umuhimu mkubwa wa kuwa na daftari la orodha ya watu wenye ulemavu, Serikali haijaweza kufanikiwa kuwaorodhesha watu wenye ulemavu katika maeneo yote ya nchi hii. Ni kwanini jitihada za Serikali kuwaorodhesha watu wote wenye ulemavu hugonga mwamba?

+

Ni kutokana na sababu mbalimbali kama vile imani potofu kwa baadhi ya jamii kama vile uchawi kwamba kumhesabu mtu ni kutaka kumroga, baadhi ya walemavu kufichwa na kutoonekana kabisa na kutumiwa kwenye imani za kishirikina, baadhi ya familia kutotaka kuwapeleka kliniki watoto wanaozaliwa wakiwa ni walemavu, wanawake wengi kuzalia (kujifungulia) nyumbani badala ya hospitali, vituo vya afya au zahanati na sababu nyinginezo.

Sheria Kiganjani
Learn More
85

Nini umuhimu wa kutoa elimu kwa umma juu ya haki na mahitaji ya watu wenye ulemavu?

+

Ni muhimu kutoa elimu kwa umma juu ya haki na mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kutokomeza ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu, walemavu wenyewe kufahamu haki zao, jamii kufahamu wajibu wake kwa watu wenye ulemavu katika jamii, kutokomeza au kuondoa imani na mitazamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu na watu wenye ulemavu wenyewe kufahamu wajibu wao katika jamii katika masuala yote ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Sheria Kiganjani
Learn More
86

Je, ni muhimu kuwa na wataalamu wenye weledi wa masuala yanayohusu watu wenye ulemavu? Kwanini?

+

Ni muhimu kuwa na wataalamu wenye weledi wa mambo yahusuyo watu wenye ulemavu kwasababu wanakuwa na mafunzo ya njia za mawasiliano kama vile kujua nukta nundu zinazotumiwa na watu wasioona kama maandishi au lugha ya alama inayotumiwa na watu wasiosikia . Mfano, vyuo mbalimbali hapa nchini kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina kozi ya lugha ya alama.Wataalamu hawa wenye weledi katika njia hizi za mawasiliano husaidia kuwatafsiria watu wengine wasioelewa njia hizi za mawasiliano. Pia, wataalamu wenye weledi wa mambo yahusuyo watu wenye ulemavu husaidia wakati wa utungaji wa sera mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi kuweka mazingira bora kwa watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
87

Kwanini ni muhimu Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya watu wenye ulemavu kukuza na kuendeleza vipaji vyao mbalimbali?

+

Ni muhimu kwasababu kama watu hawa wenye ulemavu wakiendeleza vipaji vyao, Serikali na taifa kwa ujumla tunapata kufaidika na matunda ya vipaji vyao, watu hao wenye ulemavu wanaweza kujipatia kipato na hivyo kujiendeleza wao wenyewe kiuchumi na kuacha utegemezi kwa ndugu zao, watu hao wanakuwa mfano bora kwa watu wengine wenye ulemavu na hata wasio na ulemavu na pia inasaidia kuionesha jamii kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kufanya jambo lolote kama watu wasio na ulemavu na hatimaye jamii zenye mitazamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu kuachana nayo mara moja.

Sheria Kiganjani
Learn More
88

Je, nani mwenye wajibu wa kuhakikisha kuwa mazingira ya upigaji kura ni wezeshi kwa mtu mwenye ulemavu kutimiza haki yake ya kupiga kura?

+

Ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum akishirikiana na Baraza la Taifa la Ushauri wa Huduma kwa Watu wenye Ulemavu pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Sheria Kiganjani
Learn More
89

Nini maana ya Nyenzo za kujimudu kwa mtu mwenye ulemavu?

+

Nyenzo za kujimudu kwa mtu mwenye ulemavu ni vifaa (nyenzo) vinavyomwongezea uwezo mtu mwenye ulemavu kumudu mazingira. Mfano wa nyenzo za kujimudu kwa watu wenye ulemavu ni kama vile fimbo kwa watu wasioona na baiskeli za watu wenye ulemavu wa viungo

Sheria Kiganjani
Learn More
90

Kwa mujibu wa kifungu namba 33 (3) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 ni kosa la jinai kwa mwajiri yeyote kumbagua mtu mwenye ulemavu kuhusu suala zima la ajira na adhabu yake ni faini ya shilingi milioni mbili za kitanzania au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja. Nini umuhimu wa kifungu hiki kidogo cha sheria?

+

Sababu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutunga kuweka kifungu hiki kidogo cha sheria ni kuweka mkazo na msisitizo mkubwa katika suala zima la waajiri kutowabagua watu wenye ulemavu wakati wa kutoa ajira na wakati wote. Kifungu hiki kidogo cha sheria kinawafanya waajiri katika taasisi za umma na binafsi kujitahidi kutowabagua watu wenye ulemavu kwasababu wanaogopa adhabu hiyo kali iliyowekwa na sheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
91

Je, nani ana wajibu wa kukabili matishio ya usalama wa watu wenye ulemavu kama vile tishio la kuwaua watu wenye ulemavu wa viungo?

+

Serikali inawajibu wakulinda usalama wa maisha ya watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
92

Je, Serikali ya mtaa ina wajibu gani kisheria baada ya kugundua kuwa katika mtaa au kijiji fulani ndani ya mamlaka yake kuna mtu mwenye ulemavu na hana ndugu wa kumpa msaada wowote wa kijamii?

+

Serikali ya mtaa katika mazingira hayo ina wajibu wa kumlinda na kumpa msaada mtu huyo mwenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
93

Katika hali ya kawaida, baadhi ya majengo ya umma kama vile majengo ya hospitali, shule, vyuo na ofisi za umma kwa sasa hayana mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu yanayoweza kuwawezesha kutumia kirahisi majengo hayo kama watu wengine wasio na ulemavu. Je, sheria inawapa wajibu gani wahandisi, wasanifu majengo au wajenzi wanapokuwa wanafanya ujenzi wa majengo ya umma, uchoraji wa ramani za majengo au wakati wa ukarabati wa majengo ya umma?

+

Sheria inawapa wajibu wahandisi, wasanifu majengo na watu wote wanaohusika katika ujenzi au ukarabati wa majengo ya umma kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali ili kuwawezesha kupata haki yao ya kuyatumia maeneo hayo kirahisi.

Sheria Kiganjani
Learn More
94

Mtu asiyeona hana haki kwa mujibu wa sheria kukopa kiasi chochote cha fedha kutoka katika benki ya biashara.

+

SI KWELI, kila mtu ana haki ya kukopa kiasi chochote cha fedha isipokuwa tu asipotimiza masharti ya mkopo huo.

Sheria Kiganjani
Learn More
95

Nini umuhimu wa “ubaguzi chanya” kwa watu wenye ulemavu?

+

Ubaguzi chanya kwa watu wenye ulemavu ni muhimu kwasababu huwapendelea watu wenye ulemavu na kuwapa huduma ambazo wanazistahili wao tofauti na watu wengine ambao si walemavu. Watu wenye ulemavu wanaweza kupata huduma bora zaidi kuliko watu wengine kwasababu ya kiwango cha uhitaji wao. Hivyo, sera na mipango mbalimbali inayowapendelea watu wenye ulemavu ni ya muhimu sana katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwasababu mahitaji ya watu ambao si walemavu hayawezi kufanana na mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
96

“Nini maana ya ubaguzi chanya” kwenye mambo yanayohusu haki za watu wenye ulemavu?

+

Ubaguzi chanya ni sera na vitendo mbalimbali ambavyo huwapendelea watu wenye ulemavu kuliko watu wengine wasio na ulemavu.

Sheria Kiganjani
Learn More
97

Je, ni changamoto gani wanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu wanakutana nazo wakati wa kutoa elimu juu ya haki za watu wenye ulemavu kwa jamii na watu wenye ulemavu kwa ujumla?

+

Wanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu hukutana na changamoto mbalimbali kama vile changamoto za mawasiliano kwa badhi ya watu wenye ulemavu hasa kwa maeneo ambayo hamasa na mwamko wa kuwapeleka watu wenye ulemavu katika mafunzo ya njia za mawasiliano bado uko chini na pia baadhi ya familia kuwaficha watu wenye ulemavu kutokana na imani hasi dhidi ya watu wenye ulemavu kwani baadhi ya jamii huamini kwamba kuzaa mtoto mwenye ulemavu ni nuksi na laana katika ukoo husika n.k.

Sheria Kiganjani
Learn More
98

Kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997, watu wote ni sawa na hakuna mtu yeyote anayetakiwa kubaguliwa kwa misingi yoyote. Je, Ibara hii ya Katiba kina maana gani ukihusianisha na watu wenye ulemavu nchini Tanzania?

+

Watu wenye ulemavu hawatakiwi kubaguliwa kwa namna yoyote kwa misingi ya ulemavu wao.

Sheria Kiganjani
Learn More
99

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ndiyo inayoshughulikia masuala yanayowahusu watu wenye ulemavu. Je, wizara zingine kama vile wizara inayoshughulikia masuala ya kazi na ajira na zingine zina wajibu gani kuhusu watu wenye ulemavu?

+

Wizara zingine zina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi yanayowawezesha watu wenye ulemavu kushiriki vema katika shughuli zilizopo katika wizara husika au kupata huduma zinazotolewa na wizara husika kama watu wengine. Mfano, Wizara inayohusika na kazi na ajira ina wajibu wa kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kuwafanya watu wenye ulemavu kuajiriwa na kufanya kazi ili kujipatia kipato na kujiletea maendeleo.

Sheria Kiganjani
Learn More
100

Je, kisheria ni nani mwenye wajibu wa kutoa msaada wa kijamii kwa mtu mwenye ulemavu?

+

Wote waliotajwa wana wajibu kisheria kutoa msaada wa kijamii kwa ndugu yao ambaye ana ulemavu (kifungu namba 16 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010).

Sheria Kiganjani
Learn More

Subscribe to Our News Letter

Subscribe to our newsletter to get the latest news and updates from Sheria Kiganjani

logo

Various Topics

  • The Beginning
  • Topic
  • About
  • Communicate with us
  • Article
  • Landesa

Working Hours

  • Monday - Friday
  • 08:00AM - 5:00PM
  • Saturday
  • 08:00 - 1:00PM

Call us: +255 621 900 555

Email: [email protected]

Visit us

7th Floor, Tanzanite Park Victoria Area POBOX 6622 Dar Es Salaam

Copyright © 2025 All Right Reserved Law in the palm of your hand