Legal Questions

Questions & Answers

Find answers to common legal questions and learn more about your rights

1

Ikiwa ndani ya eneo la kazi kuna kuna wawakilishi wa usalama wa afya zaidi ya mmoja, upi ni wajibu wa mwajiri kisheria?

+

Endapo kuna wawakilishi wa usalama wa afya zaidi ya mmoja katika eneo la kazi, sheria inamtaka mwajiri kuunda kamati za usalama na afya mahali pa kazi. Kamati hizi zitafanya kazi mahususi ya kuhakikisha hali ya usalama na afya mahali pa kazi na waajiriwa wako katika mazingira mazuri.

Sheria Kiganjani
Learn More
2

Kuna kazi mbalimbali viwandani au maeneo mbalimbali ya kazi ambazo hufanywa na wafanyakazi wakiwa wamesimama tu. Je, katika hali kama hii, sheria inasemaje kuhusu wakati wao wa kupumzika ndani ya saa za kazi?

+

Kwa wafanyakazi ambao wanafanya kazi wakiwa wamesimama, sheria inaelekeza kuwa viti vya kukaa vinatakiwa kuwepo ili wafanyakazi hao wakae wakati wanapopata mapumziko muda wowote wakati wa saa za kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
3

Je, maombi ya kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya mkaguzi hufikishwa kwa nani?

+

Maombi ya kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya mkaguzi huwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu ili kuona kama kuna sababu za mashiko kuruhusu rufaa hiyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
4

Mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi anatakiwa kutuma maombi ya usajili wa kiwanda chake au eneo la kazi kabla ya kuanza kazi. Je, maombi ya usajili wa kiwanda au eneo la kazi huwasilishwa kwa nani?

+

Maombi ya usajili wa kiwanda au eneo la kazi huwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu.

Sheria Kiganjani
Learn More
5

Je, mkaguzi anaweza kuwa shahidi kwenye shitaka la jinai ambalo amelianzisha yeye mwenyewe mahakamani dhidi ya mwajiri?

+

Ndiyo mkaguzi anaruhusiwa kisheria kuwa shahidi kwenye shitaka la jinai ambalo amelianzisha au amelifikisha mwenyewe mahakamani.

Sheria Kiganjani
Learn More
6

Je, ni lazima kwa mmiliki wa eneo la kazi au kiwanda kuandikisha au kusajili eneo lake la kazi au kiwanda kwa Mkaguzi Mkuu?

+

Ndiyo, sheria inamtaka mtu yeyote ambaye ni mmiliki wa eneo la kazi au kiwanda kabla ya kuanza kazi kuhakikisha anafanya usajili kwa Mkaguzi Mkuu na kama ilivyoelekezwa kisheria. Hivyo basi, kabla ya kuanza biashara au kazi husika, mmiliki huyo anapaswa kuandikisha kwa Mkaguzi Mkuu.

Sheria Kiganjani
Learn More
7

Ni kosa kwa mujibu wa sheria mtu yeyote kumzuia mkaguzi kutekeleza majukumu yake. Je, adhabu yake ni ipi pale mtu anapokutwa na hatia hiyo?

+

Adhabu yake ni kifungo cha miezi mitatu jela au faini isiyozidi shilingi milioni mbili za kitanzania au vyote kwa pamoja.

Sheria Kiganjani
Learn More
8

Je, nani anaweza kufanya uchunguzi au ukaguzi wa lifti za majengo ya kiwanda au mahali pa kazi?

+

Anayeweza kufanya uchunguzi au ukaguzi wa lifti za majengo ya kiwanda au mahali pa kazi ni mtu aliyethibitishwa kufanya hivyo na Mkaguzi Mkuu.

Sheria Kiganjani
Learn More
9

Je, kwa mujibu wa sheria, ni jambo gani ambalo mkaguzi anatakiwa kufanya baada ya kufanya uchunguzi juu ya jambo lililosababisha ugonjwa, kifo au majeraha kwa wafanyakazi eneo la kazi?

+

Baada ya kukamilisha uchunguzi, mkaguzi anatakiwa kuandika ripoti na kuikabidhi kwa Mkaguzi Mkuu kwa lengo la kushughulikiwa ipasavyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
10

Je, baada ya kutuma maombi ya kujisajili kwenye mamlaka husika. Ni uthibitisho gani mwajiri au mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi atapata kuonesha kuwa amekubaliwa na kwamba amefuata taratibu zote za kisheria?

+

Baada ya maombi kuwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu na Mkaguzi Mkuu kujiridhisha kuwa eneo husika la kazi au kiwanda kimefuata taratibu zote za kisheria atatoa Cheti Maalumu cha Usajili.

Sheria Kiganjani
Learn More
11

Je, baada ya mkaguzi kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kwa Mkaguzi Mkuu, ni hatua au maamuzi gani ambayo yanaweza kutolewa au kuchukuliwa baada ya hapo?

+

Baada ya Mkaguzi Mkuu kupokea ripoti ya uchunguzi na kujiridhisha anaweza; i. Kutoa ushauri kwa kadri inavyowezekana ii. Kutoa maelekezo ya kufanya marekebisho husika iii. Kutoa katazo la jambo fulani iv. Kulifikisha suala hilo mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe ipasavyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
12

Je, makosa ya jinai yanayofanywa chini ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanaweza kusikilizwa na kutolewa hukumu katika Mahakama ya mwanzo?

+

Hapana, kwa mujibu wa kifungu cha 87 cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, makosa yote chini ya sheria tajwa yanatakiwa kusikilizwa na kutolewa maamuzi na Mahakama ya Hakimu Mkazi au Mahakama ya Wilaya na Hakimu anayesikiliza kesi hiyo anatakiwa kuwa Hakimu Mkazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
13

Je, mwajiri anaruhusiwa kupunguza mishahara ya wafanyakazi kwasababu ya gharama mbalimbali za ukaguzi unaofanywa chini ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi au kwasababu ya gharama za vifaa vinavyonunuliwa kwa ajili ya usalama na afya ya wafanyakazi mahali pa kazi?

+

Hapana, mwajiri haruhusiwi kupunguza mishahara ya wafanyakzi kwasababu ya gharama zozote za ukaguzi unaofanywa chini ya Sheria ya Usalama Afya Mahali pa Kazi wala kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vinavyotumika kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Hii ni kwasababu Sheria inamtaka mwajiri kugharamia gharama zote hizo yeye mwenyewe na si mtu mwingine.

Sheria Kiganjani
Learn More
14

Je, mwajiri au daktari anayefanya vipimo vya afya vya wafanyakazi katika eneo la kazi anaruhusiwa kutoa siri za matokeo ya vipimo hivyo popote pale?

+

Hapana, Sheria imeweka katazo kwa daktari anayefanya vipimo vya afya ya wafanyakazi pamoja na mwajiri kutunza siri za matokeo ya vipimo hivyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
15

Sheria inamruhusu Mkaguzi Mkuu kukasimisha mamlaka yake kwa afisa yeyote. Je, Mkaguzi Mkuu anazuiwa kufanya kazi ambayo ameshaikasimisha kwa afisa mwingine mwenyewe?

+

Hapana, sheria inamruhusu Mkaguzi Mkuu kufanya kazi ile ile mwenyewe hata baada ya kuikasimisha kwa afisa yeyote.

Sheria Kiganjani
Learn More
16

Je, mwajiri anaruhusiwa kisheria kumwajiri mtu katika shughuli za kilimo katika maeneo ambayo ni hatarishi kama vile yenye wanyama au wadudu wakali bila kujali matatizo anayoweza kuyapata mwajiriwa huyo?

+

Hapana, Sheria kupitia kifungu cha 65 inamtaka mwajiri anayemwajiri mtu kufanya kazi katika shughuli za kilimo kuhakikisha kuwa mwajiriwa huyo hafanyi kazi katika mazingira hatarishi kama vile maeneo ya wanyama wakali au matumizi ya madawa yanayoweza kumsababishia madhara ya kiafya.

Sheria Kiganjani
Learn More
17

Je, mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi anaweza kuamua kwamba waajiriwa (wafanyakazi) wake watumie vifaa au kemikali zenye sumu wakati kazi hiyo hiyo inaweza kufanywa kwa kutumia vifaa au kemikali zisizo na sumu?

+

Hapana, Sheria kupitia kifungu cha 67 inaelekeza wazi kuwa matumizi ya vifaa au kemikali zenye sumu litakuwa ni chaguo la mwisho, yaani pale ambapo kazi hiyo haiwezi kufanyika kwa kutumia vifaa au kemikali zingine zisizo na sumu.

Sheria Kiganjani
Learn More
18

Mkaguzi ana mamlaka ya kisheria kumhoji mwajiri au mwajiriwa mahali pa kazi na kupewa majibu ipasavyo. Je, mwajiri au mwajiriwa ana wajibu wa kujibu maswali au kutoa ushahidi ambao unaweza kumtia hatiani yeye mwenyewe?

+

Hapana, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi inampa haki mwajri au mwajiriwa anayehojiwa na mkaguzi kutojibu maswali au kutoa ushahidi ambao unaweza kumtia hatiani yeye mwenyewe.

Sheria Kiganjani
Learn More
19

Sheria chini ya kifungu namba 4 ya sheria ya usalama mahali pa kazi inampa mamlaka Waziri wa Kazi kuteua Mkaguzi Mkuu. Eleza kwa ufupi majukumu ya Mkaguzi Mkuu.

+

i. Kufanya ukaguzi mahali pa kazi kujiridhisha kama taratibu na kanuni zinafuatwa ipasavyo. ii. Kuhifadhi rejesta ya viwanda iii. Kuhifadhi nyaraka zote ambazo zinahusiana na viwango vya usalama na afya kama ilivyoelekezwa kwenye sheria, kanuni na miongozi. iv. Kuhifadhi nyaraka zote ambazo zinatakiwa kusajiliwa chini ya sheria v. Kuteua wakaguzi ambao watapewa cheti maalumu na wenye mamlaka kisheria kutembelea na kukagua sehemu ya kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
20

Kwa mujibu wa sheria, wakaguzi walioteuliwa na Mkaguzi Mkuu wanayo majukumu kisheria. Elezea majukumu na mamlaka waliyo nayo wakaguzi hao kwa mujibu wa sheria.

+

i. Kuingia na kufanya ukaguzi wakati wa mchana au usiku kwenye eneo lolote la kazi linalotambulika kisheria bila hata kutoa taarifa ii. Kuingia na kukagua sehemu yoyote ambayo kuna sababu za kuamini ni eneo la kazi ambapo vitu vyenye asili ya mlipuko vinahifadhiwa au kutumika iii. Kumtaka mtu yeyote anayekutwa eneo la kazi kuwapatia taarifa wanayoihitaji pale ambapo mtu huyo ana mamlaka ya kutoa taarifa iv. Kutekeleza majukumu mengine yanayohusisha ukaguzi wa mashine au vitendea kazi vyote eneo la kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
21

Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa kazi imeipa nguvu OSHA kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Eleza shughuli mbalimbali ambazo OSHA kama wakala wa serikali hujishughulisha nazo

+

i. Kusajili sehemu za kazi ii. Kufanya ukaguzi wa jumla iii. Kutathmini hatari zilizopo mahali pa kazi iv. Kufanya mapitio ya michoro na majenzi ya sehemu za kazi v. Kufanya uchunguzi wa afya na magonjwa kulingana na kazi husika mahali pa kazi vi. Kufanya uchunguzi wa ajali zinazotokea sehemu ya kazi vii. Kufanya tathmini ya athari ya kimazingira viii. Kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi

Sheria Kiganjani
Learn More
22

OSHA kama taasisi inayoshughulikia masuala yote yanayohusu usalama wa afya mahali pa kazi inayo majukumu ya msingi. Elezea majukumu manne ya msingi ya OSHA.

+

i. Kusimamia utekelezaji wa Sheria namba 5 ya mwaka 2003 ya Usalama wa afya mahali pa kazi. ii. Kuishauri serikali kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, kuhusiana na sera, kanuni na miongozo mbalimbali ya usimamizi wa usalama na afya nchini. iii. Kuongeza uelewa miongoni mwa wadau kuhusiana na masuala ya Usalama na Afya kwa kutoa mafunzo mbalimbali ikiwemo kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau. iv. Kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na masuala ya usalama na afya katika sehemu za kazi ili kuweza kushauri serikali namna bora ya kutekeleza sera tajwa.

Sheria Kiganjani
Learn More
23

Sheria imeweka katazo kwenye uteuzi wa wakaguzi. Eleza katazo lililowekwa kisheria kwa mtu kuteuliwa kuwa mkaguzi.

+

i. Mtu yeyote ambaye anamiliki kiwanda au eneo lolote la kazi haruhusiwi kuteuliwa kuwa mkaguzi. ii. Mtu yeyote anayenufaika na kiwanda au eneo la kazi moja kwa moja haruhusiwi kuwa mkaguzi. iii. Pia mwajiriwa wa kiwandani au eneo la kazi haruhusiwi kuteuliwa kuwa mkaguzi.

Sheria Kiganjani
Learn More
24

Sheria inaelekeza kuwa kila eneo la kazi lazima kuwe na Mwakilishi wa Usalama wa Afya, je ni idadi gani inahitajika kisheria?

+

Ikiwa ni duka au ofisi, Mwakilishi wa Usalama wa Afya awe mmoja kwa wafanyakazi miamoja (100) au chini ya hapo. Ikiwa ni kiwandani, angalau anahitajika Mwakilishi wa Usalama wa Afya mmoja kwa kila wafanyakazi hamsini (50) wa kiwanda.

Sheria Kiganjani
Learn More
25

Nini kinapaswa kufanyika ikiwa idadi ya wakilishi wa usalama wa afya ni ndogo kuliko ile iliyowekwa kisheria?

+

Kama ikitokea hali hiyo, Mkaguzi Mkuu atamwandikia notisi ya maandishi mwajiri husika akimtaka kuwa na wawakilishi wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
26

Je, mtu aliyepewa uthibitisho wa kujenga kiwanda kutoka kwa Mkaguzi Mkuu baada ya kuwasilisha michoro yake anahitaji kufanya nini tena baada ya kuanza zoezi la ujenzi wa kiwanda husika?

+

Kifungu cha 22 (1) cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kinamtaka mtu baada ya kupewa uthibitisho kujenga kiwanda, kumwita Mkaguzi Mkuu kwa ajili ya kufanya ukaguzi mwingine wa zoezi la ujenzi wa kiwanda hicho.

Sheria Kiganjani
Learn More
27

OSHA ni taasisi ambayo ni wakala wa Serikali na ina wajibu wa kushughulikia mambo yote yanayohusiana na usalama na afya mahali pa kazi. Taja kirefu cha OSHA

+

Kirefu cha OSHA ni “Occupational Safety and Health Authority”.

Sheria Kiganjani
Learn More
28

Kisheria, kiwanda au mahali pa kazi ambapo huhusisha matumizi ya umeme hutakiwa kukaguliwa kila mwaka na cheti cha uthibitisho kutolewa. Je, mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi anatakiwa kufanya kitu gani mwezi mmoja kabla ya kuisha kwa muda wa cheti cha mwaka uliopita?

+

Kisheria mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi anatakiwa kutoa taarifa kwa Mkaguzi Mkuu mwezi mmoja kabla ya kuisha kwa muda wa cheti cha mwaka uliopita.

Sheria Kiganjani
Learn More
29

Je, yapi ni madhara kisheria ikiwa mmiliki ataanzisha kiwanda au eneo la kazi na kushindwa kutuma maombi ya usajili kwa Mkaguzi Mkuu?

+

Kutojisajili ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria. Adhabu ya kosa hili inaweza kuwa faini isiyopungua shilingi milioni moja na isiyozidi milioni tano au kifungo jela kisichozidi miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja. Iikiwa ataendelea na kazi pasi na kuwa na cheti hicho hata baada ya kulipa faini au kutumikia kifungo jela, sheria inatoa adhabu ya faini ya kiasi cha shilingi laki moja kwa kila siku tangu kosa hilo liendelee.

Sheria Kiganjani
Learn More
30

Ni taasisi gani inayoshughulikia masuala yote yanayohusu usalama wa afya mahali pa kazi nchini Tanzania?

+

Kwa mujibu wa sheria ya usalama wa afya mahali pa kazi taasisi ya OSHA ndiyo wakala wa Serikali anayetambulika kisheria na mwenye wajibu wa kushughulikia masuala yote yanayohusiana na usalama wa afya mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
31

Je, leseni ya utii hutolewa kwa kipindi cha muda gani?

+

Leseni ya utii hutolewa kwa kipindi cha muda wa mwaka mmoja (yaani miezi kumi na mbili).

Sheria Kiganjani
Learn More
32

Nini maana ya Leseni ya utii?

+

Leseni ya utii ni cheti au leseni ambayo mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi anapewa kwa kipindi cha muda fulani baada ya kuwa ametimiza matakwa yote ya msingi ya kisheria yanayohusiana na usalama na afya mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
33

Je, nini kinatakiwa kufanyika pale ambapo mwajiriwa amepata ajali na kujeruhiwa na baada ya kupata huduma ya kwanza na kuhitaji huduma zaidi?

+

Majeruhi anapohitaji huduma zaidi baada ya kupatiwa huduma ya kwanza, sheria inaelekeza kuwa huduma ya usafiri wa kuaminika itolewe na kumfikisha katika kituo cha utoaji wa huduma za afya.

Sheria Kiganjani
Learn More
34

Kuna wizara mbalimbali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, mambo ya kazi yako chini ya wizara gani? Itaje kwa usahihi.

+

Mambo ya kazi yako chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu).

Sheria Kiganjani
Learn More
35

Kila kiwanda au mahali pa kazi panatakiwa kusajiliwa kwa Mkaguzi Mkuu. Je, ni wakati gani ambapo mmiliki wa kiwanda anatakiwa kutuma maombi ya usajili wa kiwanda au mahali pa kazi?

+

Maombi ya usajili wa kiwanda au mahali pa kazi yanatakiwa kufanywa kabla ya kuanza kazi husika kiwandani hapo au mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
36

Je, Mkaguzi Mkuu wa Usalama na Afya mahali pa kazi hupatikana kwa njia gani?

+

Mkaguzi Mkuu wa Usalama na Afya mahali pa kazi hupatikana kwa njia ya kuteuliwa. Mkaguzi Mkuu huteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
37

Mkaguzi Mkuu anaweza kutoa maamuzi dhidi ya mmiliki wa kiwanda au eneo lolote la kazi. Je, ikiwa mmiliki huyo wa kiwanda hajaridhishwa na maamuzi ya Mkaguzi Mkuu, anaweza kufanya nini ili apate haki yake?

+

Mmiliki wa kiwanda ambaye hajaridhishwa na maamuzi ya Mkaguzi Mkuu anaweza kukata rufaa dhidi ya maamuzi hayo.

Sheria Kiganjani
Learn More
38

Je, mmiliki wa kiwanda anapobadilika, nini kinatakiwa kufanyika na ni ndani ya muda gani?

+

Mmiliki wa kiwanda anapobadilika, mmiliki huyo mpya ana wajibu wa kumtaarifu Mkaguzi Mkuu juu ya mabadiliko hayo na anatakiwa kufanya hivyo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja baada ya mabadiliko hayo.

Sheria Kiganjani
Learn More
39

Je, mmiliki wa kiwanda kilichokuwa kimesajiliwa au mahali pa kazi ana wajibu gani kisheria baada ya kufunga kiwanda chake au mahali pake pa kazi na kuacha kufanya kazi?

+

Mmiliki wa kiwanda kilichokuwa kimesajiliwa au mahali pa kazi ana wajibu kisheria pale anapotaka kufunga na kuacha kufanya kazi kumtaarifu Mkaguzi Mkuu kuwa amefunga kiwanda na kwamba ameacha kufanya kazi husika.

Sheria Kiganjani
Learn More
40

Mwajiri au mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi anatakiwa kabla ya kuanza kazi husika atume maombi ya usajili kwa maandishi kwa Mkaguzi Mkuu. Je, ni vitu gani vinahitajika kuwepo katika maombi hayo kwa mujibu wa sheria?

+

Moja, jina la mmiliki huyo Mbili, Anwani na mahali kilipo kiwanda hicho au mahali pa kazi Tatu, Aina ya kazi inayofanyika au itakayokuwa inafanyika mahali hapo au kiwandani hapo Nne, Idadi ya waajiriwa au watu wanaotarajiwa kuajiriwa

Sheria Kiganjani
Learn More
41

Leseni ya utii inakuwa na vitu mbalimbali. Taja vitu vitano ambavyo vinatakiwa kuwa kwenye leseni ya utii.

+

Moja, Jina la mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi Mbili, Anwani na mahali kiwanda kilipo au mahali pa kazi Tatu, Aina ya kazi inayofanywa kiwandani hapo au mahali pa kazi Nne, Muda wa uhalali wa leseni hiyo (kabla ya kuisha muda wake) Tano, Jina la afisa aliyetoa leseni hiyo

Sheria Kiganjani
Learn More
42

Taja majukumu manne ya Mwakilishi wa Usalama wa Afya chini ya sheria.

+

Moja, kufanya mapitio ya hatua na tahadhari zilizochukuliwa na kiwanda eneo la kazi kuhakikisha usalama wa afya mahali pa kazi Mbili, Kuweka bayana hatari zilizopo eneo la kazi na ajali zinazotokea kiwandani au eneo la kazi. Tatu, Kushirikiana na mwajiri katika kuchunguza chanzo cha ajali katika eneo la kazi Nne, Kuchunguza malalamiko yanayoletwa na mwajiriwa kuhusiana na usalama wa afya ya mwajiriwa eneo la kazi. Tano, Kumsaidia mkaguzi ikiwa atafika katika eneo husika kwa ajili ya ukaguzi

Sheria Kiganjani
Learn More
43

Kuna wadau mbalimbali wanaohusika na mambo yahusuyo usalama na afya mahali pa kazi. Taja wadau watano wa mambo yahusuyo usalama na afya mahali pa kazi hapa Tanzania na hata duniani kwa ujumla.

+

Moja, Taasisi ya OSHA Mbili, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Tatu, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini Tanzania (TUCTA) Nne, Shirika la Kazi Duniani (ILO)

Sheria Kiganjani
Learn More
44

Je, ni nani anaweza kuchaguliwa kuwa Mwakilishi wa Usalama na Afya katika eneo la kazi?

+

Mtu anayeweza kuchagaliwa kuwa Mwakilishi wa Usalama wa Afya katika eneo la kazi ni mwajiriwa yeyote aliyeajiriwa kwa ajira ya kudumu na anaye elewa vizuri mazingira na shughuli zote zinazofanywa katika eneo husika.

Sheria Kiganjani
Learn More
45

Je, pale ambapo waajiriwa wanafanya kazi kwenye kiwanda au mahali pa kazi ambapo panahusisha utoaji wa vumbi, moshi na vitu vingine vya aina hiyo kwa kiwango ambacho kinaweza kuwa hatari sana kwa afya za waajiriwa, mwajiri anakuwa na wajibu gani kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Afya na Mahali pa Kazi?

+

Mwajiri anakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa hatua zote zinazowezekana zinachukuliwa kwa ajili ya kuwakinga waajiriwa kuvuta moshi, vumbi au vitu vingine vya aina hiyo, kuhakikisha kuwa moshi au vumbi haiingii ndani ya chumba cha kufanyia kazi na kuhakikisha kuwa mtu yeyote haruhusiwi kula chakula au kunywa kinywaji akiwa ndani ya eneo hilo lenye moshi au vumbi hiyo ili isiingie kwenye chakula au kinywaji hicho.

Sheria Kiganjani
Learn More
46

Ikiwa mwajiri au mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi hajaridhishwa na maamuzi ya Mkaguzi Mkuu anaweza kukata rufaa. Je, mwajiri anatakiwa kukata rufaa ndani ya muda gani baada ya hukumu kutolewa?

+

Mwajiri anatakiwa kukata rufaa ndani ya siku thelathini (30) baada ya maamuzi hayo kutolewa.

Sheria Kiganjani
Learn More
47

Ikiwa mwajiri ana eneo la kazi na ana wafanyakazi zaidi ya ishirini (20), sheria inamtaka kutekeleza baadhi ya mambo yatakayosaidia kuimarisha usalama wa afya mahali pa kazi. Taja jambo moja tu ambalo mwajiri anatakiwa kufanya.

+

Mwajiri anatakiwa kumteua mtu anayejulikana kama “Mwakilishi wa Usalama wa Afya” katika eneo husika la kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
48

Je, nani mwenye wajibu kwa mujibu wa sheria kuhakikisha kuwa vyombo vyote vinavyohifadhi kemikali vinakuwa na nembo inayoonesha hivyo wakati wote?

+

Mwajiri au mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi ndiye mwenye wajibu kisheria chini ya kifungu cha 75 (2) kuhakikisha kuwa vyombo vyote vinavyohifadhi kemikali vinakuwa na nembo zinazotofautisha chombo kimoja chenye kemikali fulani na chombo kingine chenye kemikali nyingine.

Sheria Kiganjani
Learn More
49

Je, nani mwenye mamlaka ya kupanga kiasi cha ada ya usajili wa viwanda au mahali pa kazi?

+

Mwenye mamlaka ya kupanga kiasi cha ada ya usajili wa viwanda au mahali pa kazi ni Waziri mwenye dhamana ya mambo ya kazi baada ya kushauriana na Waziri wa Fedha na Mipango.

Sheria Kiganjani
Learn More
50

Je, nani mwenye wajibu kisheria kuhakikisha kuwa ngazi, kuta na sehemu mbalimbali za majengo ya kiwanda au mahali pa kazi zinakuwa katika hali salama kwa ajili ya matumizi ya wafanyakazi mahali pa kazi?

+

Mwenye wajibu kisheria kuhakikisha kuwa ngazi na kuta za majengo ya kiwanda au mahali pa kazi zinakuwa katika hali salama kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi ni mwajiri au mmiliki wa kiwanda au mahali husika pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
51

Je, uthibitisho wa michoro ya ujenzi wa kiwanda unahitaji malipo au ada ya aina yoyote kisheria?

+

Ndiyo, kifungu cha 21 (3) (a) cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kinaeleza kuwa mtu huyo anayehitaji uthibitisho wa michoro yake anatakiwa kulipa ada itakayopangwa kwa ajili ya uthibitisho wa michoro hiyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
52

Je, Mkaguzi Mkuu anapaswa kwa mujibu wa sheria kutoa sababu za kukataa kutoa uthibitisho wa michoro ya majengo ya kiwanda baada ya kuwasilishwa kwake na mtu anayetarajia kufanya ujenzi wa kiwanda?

+

Ndiyo, kwa mujibu wa kifungu cha 21 (2) (b) cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Mkaguzi Mkuu anatakiwa kutoa sababu za kukataa kuthibitisha michoro hiyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
53

Je, baada ya rufaa dhidi ya maamuzi ya Mkaguzi Mkuu kuwasilishwa kwa waziri mwenye dhamana, Mkaguzi Mkuu ana haki ya kusikilizwa?

+

Ndiyo, Mkaguzi ana haki ya kusikilizwa wakati wa rufaa iliyokatwa na mmiliki wa kiwanda dhidi ya maamuzi ya Mkaguzi Mkuu.

Sheria Kiganjani
Learn More
54

Je, mkaguzi ana mamlaka ya kumwita mwajiriwa mstaafu au aliyefukuzwa kazi na kumhoji kuhusu mambo yahusuyo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi?

+

Ndiyo, mkaguzi ana mamlaka ya kumwita mwajiriwa mstaafu au aliyefukuzwa kazi na kumhoji juu ya mambo mbalimbali yahusuyo usalama na afya katika kiwanda hicho au mahali pa kazi ambapo alikuwa ni mwajiriwa wake (kifungu cha 6 (1) (j)).

Sheria Kiganjani
Learn More
55

Je, mkaguzi ana uwezo wa kumtoza faini mwajiri anayekutwa na kosa chini ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi bila hata kumfikisha mahakamani kwa ajili ya hatua za kisheria?

+

Ndiyo, mkaguzi ana uwezo wa kumtoza faini mwajiri anayekutwa na kosa chini ya sheria bila kumfikisha mahakamani. Hii ni kwa makosa kama vile kumzuia mkaguzi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kushindwa kusajili kiwanda au mahali pa kazi na kuendelea kufanya kazi bila kusajiliwa, kuendelea na ujenzi wa kiwanda baada ya michoro kuthibitishwa bila kumwita Mkaguzi Mkuu kwa ajili ya ukaguzi mwingine, ukosefu wa vifaa vya kuzima moto, ukosefu wa sanduku la huduma ya kwanza lenye vifaa maalumu kwa ajili ya huduma ya kwanza mahali pa kazi, ukosefu wa vyoo mahali pa kazi, kushindwa kutoa taarifa kwa Mkaguzi Mkuu baada ya kufunga biashara au kuacha kuendelea na kazi na kadhalika. Mwajiri anaweza kutozwa faini moja kwa moja na mkaguzi bila hata kwenda mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
56

Je, Mkaguzi Mkuu ana mamlaka ya kumsimamisha mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi kutoendelea na kazi kwa muda pale anapojiridhisha kuwa hajatii matakwa ya msingi katika Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi?

+

Ndiyo, Mkaguzi Mkuu ana mamlaka ya kumsimamisha mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi kutoendelea na kazi kwa muda pale anapojiridhisha kuwa mwajiri huyo hajatii matakwa ya sheria kuhusu usalama na afya mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
57

Je, Mkaguzi Mkuu ana mamlaka ya kuuliza taasisi zingine za kiutawala kuhusu usahihi wa taarifa zilizotolewa na mwajiri katika maombi ya usajili?

+

Ndiyo, Mkaguzi Mkuu ana mamlaka ya kuuliza taasisi zingine za kiutawala kuhusu usahihi wa taarifa zilizotolewa na mwajiri katika maombi ya usajili wa kiwanda au mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
58

Je, Mkaguzi Mkuu anapokataa kufanya usajili baada ya kupokea maombi ya usajili ana wajibu wa kutoa sababu za kukataa huko?

+

Ndiyo, Mkaguzi Mkuu anapokataa kufanya usajili wa kiwanda au mahali pa kazi baada ya kupokea maombi ya usajili ana wajibu wa kutoa sababu za kukataa huko kwa maandishi.

Sheria Kiganjani
Learn More
59

Je, Mkaguzi Mkuu anaruhusiwa kisheria kukasimisha mamlaka yake yoyote kwa afisa yeyote?

+

Ndiyo, Mkaguzi Mkuu anaruhusiwa kukasimisha mamlaka yake kwa afisa yeyote.

Sheria Kiganjani
Learn More
60

Je, mtu yeyote ana haki ya kutoa taarifa kwa Mkaguzi Mkuu pale anapoona kuwa mwajiri au mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi anafanya mambo ambayo yako kinyume na Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi?

+

Ndiyo, mtu yeyote anaweza kutoa taarifa kwa Mkaguzi Mkuu au mkaguzi yeyote pale anapoona kuwa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi inavunjwa.

Sheria Kiganjani
Learn More
61

Je, mwajiri ana wajibu wa kutoa au kuhakikisha kuwa waajiriwa wake wanapata mafunzo, maelezo, maagizo na usimamizi ili kudumisha usalama na afya katika mahali pa kazi?

+

Ndiyo, mwajiri ana wajibu huo wa kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanapata mafunzo, maagizo, maelezo na usimamizi kuhusu usalama na afya mahali pa kazi kwa ajili ya kuwalinda dhidi ya hatari mbalimbali mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
62

Je, mwajiri ana wajibu wa kusaini fomu maalumu baada ya ukaguzi kufanywa kwenye mahali pake pa kazi?

+

Ndiyo, Mwajiri ana wajibu wa kusaini ripoti ya ukaguzi ambayo huwa kwenye fomu maalumu.

Sheria Kiganjani
Learn More
63

Je, mwajiri ana wajibu wa kuandaa mazingira safi na wezeshi kwa ajili ya waajiriwa kufua mavazi yao hasa yale ambayo hawajavaa wakati wa kazi?

+

Ndiyo, mwajiri ana wajibu wa kuweka mazingira wezeshi na salama kwa ajili ya shughuli za ufuaji wa nguo na mavazi mengine kiwandani kulingana na aina ya kazi yenyewe.

Sheria Kiganjani
Learn More
64

Je, mwajiri ana wajibu wa kuandaa mazingira safi na wezeshi kwa ajili ya waajiriwa kufua mavazi yao hasa yale ambayo hawajavaa wakati wa kazi?

+

Ndiyo, mwajiri ana wajibu wa kuweka mazingira wezeshi na salama kwa ajili ya shughuli za ufuaji wa nguo na mavazi mengine kiwandani kulingana na aina ya kazi yenyewe.

Sheria Kiganjani
Learn More
65

Je, mwajiri au mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi ana haki ya kumwomba mkaguzi cheti kinachothibitisha kuwa yeye ni mkaguzi kabla hajamruhusu kuingia na kufanya ukaguzi?

+

Ndiyo, mwajiri au mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi ana haki ya kumwomba cheti mtu yeyote anayejitambulisha kama mkaguzi ili kujiridhisha kama mtu huyo ni mkaguzi kweli kisheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
66

Je, mwajiriwa ana haki ya kutoa taarifa kwa mwajiriwa wake pale anapoona kuwa mazingira anayofanyia kazi si salama kutokana na hali yoyote?

+

Ndiyo, mwajiriwa ana haki ya kutoa taarifa kwa mwajiri pale anapoona kuwa mazingira anayofanyia kazi kiwandani au mahali pa kazi si salama kwake.

Sheria Kiganjani
Learn More
67

Je, ni lazima kwa mwajiri kuwapatia waajiri vifaa vya kujikinga na hatari pale ambapo waajiri wanafanya kazi inayohusisha vifaa au mazingira yanayoweza kusababisha majeraha au ajali yoyote?

+

Ndiyo, ni lazima kisheria kwa mwajiri kuwapatia waajiriwa vifaa vya kujikinga na hatari popote pale inapowezekana kama waajiriwa hao wanafanya kazi katika mazingira ambayo wakati wowote yanaweza kusababisha ajali au majeraha.

Sheria Kiganjani
Learn More
68

Je, ni lazima kwa mujibu wa sheria eneo la kazi kuwa na sanduku la huduma ya kwanza?

+

Ndiyo, ni lazima kwa mujibu wa sheria kila eneo la kazi kuwa na sanduku la huduma ya kwanza lenye viwango vinavyotakiwa na lenye vifaa vyote vya muhimu kwa ajili ya utoaji wa huduma ya kwanza.

Sheria Kiganjani
Learn More
69

Je, ni lazima kuweka notisi katika kila chumba cha kazi inayoonesha mtu mwenye sanduku la huduma ya kwanza?

+

Ndiyo, sheria inaelekeza kuwa ni lazima kuweka notisi katika kila chumba cha kazi inayoonesha jina la mtu mwenye sanduku la huduma ya kwanza kwa wakati fulani.

Sheria Kiganjani
Learn More
70

Je, mwajiri au mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi ana wajibu wa kuweka mazingira sawa kwa ajili ya kuwawezesha waajiriwa kufua mavazi yao?

+

Ndiyo, sheria inaelekeza kuwa waajiriwa wanatakiwa kuwekewa mazingira yote wezeshi kwa ajili ya kufua mavazi yao kadri iwezekanavyo.

Sheria Kiganjani
Learn More
71

Waajiriwa wanaweza kufanyiwa vipimo vya afya ili kujua hali zao za afya katika eneo la kazi?

+

Ndiyo, sheria inaelekeza kuwa wafanyakazi (waajiriwa) wanaweza kufanyiwa vipimo vya afya wakati wowote.

Sheria Kiganjani
Learn More
72

Je, Waziri wa Kazi ana mamlaka ya kutoa maamuzi tofauti na yale ya Mkaguzi Mkuu?

+

Ndiyo, Sheria inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana kukubaliana au kutokubaliana na maamuzi yaliyotolewa na Mkaguzi Mkuu. Hivyo, Waziri anaweza kutoa maamuzi tofauti na yale yaliyotolewa na Mkaguzi Mkuu.

Sheria Kiganjani
Learn More
73

Je, Mkaguzi Mkuu anaweza kukataa kuthibitisha michoro ya majengo ya kiwanda au mahali pa kazi iliyowasilishwa kwake kwa ajili ya kupata uthibitisho?

+

Ndiyo, sheria inamruhusu Mkaguzi Mkuu kukataa kutoa uthibitisho wa michoro ya majengo ya kiwanda au mahali pa kazi baada ya kuwasilishwa kwake.

Sheria Kiganjani
Learn More
74

Je, ni lazima kwa mkaguzi yeyote kutoa na kuonyesha cheti chake baada ya kuombwa kufanya hivyo anapofika mahali pa kazi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake?

+

Ndiyo, sheria inamtaka mkaguzi yeyote kutoa na kuonesha cheti chake baada ya kuombwa kufanya hivyo kabla ya kuanza zoezi la ukaguzi wa kiwanda au mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
75

Mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi anatakiwa kutuma maombi ya usajili wa kiwanda au mahali pa kazi kabla ya kuanza kazi husika. Je, usajili huo unahitaji malipo ya aina yoyote?

+

Ndiyo, sheria inamtaka mmiliki wakati wa kutuma maombi ya usajili kuambatanisha na ada ya usajili inayohitajika kwa mujibu wa maelekezo.

Sheria Kiganjani
Learn More
76

Je, mtu anayetarajia kujenga kiwanda au mahali pa kazi anapaswa kuwasilisha michoro ya jengo au majengo ya kiwanda anachotarajia kujenga kwa ajili ya kupata uthibitisho wa Mkaguzi Mkuu?

+

Ndiyo, Sheria inamtaka mtu yeyote anayetarajia kujenga kiwanda au mahali pa kazi kuwasilisha michoro ya kiwanda anachotarajia kujenga kwa Mkaguzi Mkuu kwa ajili ya uthibitisho.

Sheria Kiganjani
Learn More
77

Je, njia ya kufikia na kutoka kiwandani au mahali pa kazi inatakiwa kuwa salama na bila hatari kwa ajili ya matumizi ya waajiriwa na watu wote?

+

Ndiyo, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi inamtaka mwajiri au mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi kuhakikisha kuwa njia ya kuingilia na kutokea mahali pa kazi inakuwa salama bila hatari kwa ajili ya matumizi ya wafanyakazi wake na watu wote.

Sheria Kiganjani
Learn More
78

Je, Waziri mwenye dhamana ya mambo ya kazi ana mamlaka ya kuwataka waajiriwa katika kiwanda au mahali pa kazi kupimwa afya baada ya kuonekana kuwa kuna ugonjwa fulani umejitokeza na inaaminika kuwa waajiriwa hao wanaweza kuwa wameupata ugonjwa huo kutokana na asili ya kazi yao kiwandani au mahali hapo pa kazi?

+

Ndiyo, Waziri mwenye dhamana ya kazi ana mamlaka ya kuwataka waajiriwa wowote wakati wowote kupimwa afya pale anapoamini au kuona kuwa kuna uwezekano wa kuwa wamepata ugonjwa wa aina yoyote.

Sheria Kiganjani
Learn More
79

Je, ni wajibu wa nani kuhakikisha kuwa mashine zote za kazi kiwandani au mahali pa kazi ziko salama kwa ajili ya matumizi ya waajiriwa?

+

Ni wajibu wa mwajiri au mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi kuhakikisha kuwa mashine zote za kazi kiwandani au mahali pa kazi ziko salama kwa ajili ya matumizi ya waajiriwa.

Sheria Kiganjani
Learn More
80

Je, upi ni wajibu wa mwajiri pale ambapo kazi inayofanywa na waajiriwa kiwandani hapo au mahali pa kazi inahusisha vifaa vya hatari au madawa yoyote yanayoweza kusababisha hatari muda wowote?

+

Pale ambapo waajiriwa wanafanya kazi inayohusisha matumizi ya vifaa ambavyo vinaweza kusababisha hatari wakati wowote au madawa ambayo ni hatari, mwajiriwa anakuwa na wajibu kuhakikisha kuwa uchunguzi au tathmini ya hatari inafanyika kila mwaka au wakati wowote inapoonekana kuwa ni sahihi kufanya hivyo na pia mwajiri anatakiwa kuwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu au mkaguzi yeyote ushahidi unaothibitisha kuwa tathmini hiyo imefanyika anapoombwa kufanya hivyo (kifungu cha 60).

Sheria Kiganjani
Learn More
81

Nini maana ya rejesta ya viwanda na mahali pa kazi?

+

Rejesta ya viwanda na mahali pa kazi ni daftari ambalo hutunza taarifa za waajiri au wamiliki wa viwanda na mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
82

Je, baada ya Mkaguzi Mkuu kuruhusu maombi ya rufaa yaliyofanywa na mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi, rufaa inawasilishwa kwa nani?

+

Rufaa huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ya mambo ya kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
83

Lifti za majengo zinapaswa kukaguliwa ipasavyo kwani kama zisipokaguliwa huweza kusababisha madhara kwa usalama wa watumiaji mahali pa kazi. Je, lifti za majengo ya kiwandani au mahali pa kazi zinapaswa kufanyiwa ukaguzi au uchunguzi angalau mara ngapi ndani ya muda gani?

+

Sheria inaelekeza kuwa lifti za majengo zinapaswa kukaguliwa au kufanyiwa uchunguzi walau mara moja kwa kila miezi sita.

Sheria Kiganjani
Learn More
84

Je, mkaguzi baada ya kuwa ameteuliwa na Mkaguzi Mkuu kufanya kazi za ukaguzi chini ya sheria, anatakiwa kupewa nini kama uthibitisho wa uteuzi wake kama mkaguzi?

+

Sheria inaelekeza kuwa mkaguzi anyeteuliwa anatakiwa kupatiwa cheti kinachothibitisha kuwa yeye ni mkaguzi kwa mujibu wa sheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
85

Je, sheria inasemaje kuhusu uwepo wa chumba cha kubadilishia mavazi kwa ajili ya waajiriwa katika eneo la kazi?

+

Sheria inaelekeza kuwa ni lazima kuwe na vyumba maalumu kwa ajili ya waajiriwa kubadilishia mavazi na vyumba hivyo vya kubadilishia mavazi viwe tofauti kwa kila jinsi.

Sheria Kiganjani
Learn More
86

Je, mwajiri mwenye wafanyakazi wa jinsi tofauti (yaani wa kike na wa kiume) anaweza kuamua kuwajengea choo kimoja?

+

Sheria inaelekeza kuwa ni lazima mwajiri atenge vyoo kwa ajili ya waajiriwa wa kike na vyoo vingine kwa ajili ya waajiriwa wa kiume.

Sheria Kiganjani
Learn More
87

Je, sheria inasemaje kuhusu uwepo wa mtu mwenye mafunzo ya utoaji wa huduma ya kwanza katika mahali pa kazi.?

+

Sheria inaeleza kuwa anatakiwa kuwepo mtu mwenye mafunzo ya utoaji wa huduma ya kwanza katika mahali pa kazi na anatakiwa kuwepo mahali pa kazi wakati wote wa saa za kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
88

Katika hali ya kawaida, kuna gharama ambazo zinajitokeza wakati wafanyakazi wanapofanyiwa vipimo vya afya. Je, nani anawajibika na gharama hizi?

+

Sheria inaeleza wazi kuwa gharama zote wakati wa kufanya vipimo vya afya zinakuwa juu ya mwajiri.

Sheria Kiganjani
Learn More
89

Je, nani mwenye wajibu wa kugharamia gharama zote za uchunguzi unaofanywa na mkaguzi kuhusu chanzo cha kifo, ugonjwa au majeraha ya mfanyakazi au wafanyakazi?

+

Sheria inaeleza wazi kuwa gharama zote za uchunguzi zinagharamiwa na mmiliki wa kiwanda au mtu anayesimamia eneo hilo la kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
90

Je, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi inasemaje kuhusu mkaguzi wa usalama wa afya mahali pa kazi anapofika kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kuzuiwa kufanya hivyo?

+

Sheria inaeleza wazi kuwa ni kosa la jinai mtu yeyote kumzuia mkaguzi kutekeleza majukumu yake.

Sheria Kiganjani
Learn More
91

Je, sheria inampa wajibu gani mwajiri yeyote mwenye wafanyakazi (waajiriwa) zaidi ya wanne kuhusu suala la uwepo wa sera ya afya na usalama wa wafanyakazi kiwandani au mahali pa kazi?

+

Sheria inampa wajibu mwajiri mwenye waajiriwa zaidi ya wanne kuandaa kwa maandishi sera ya afya na usalama wa wafanyakazi, kuandaa miongozo ya namna ya kutekeleza sera hiyo, kubandika au kuonyesha sera hiyo maeneo yote ya wazi na kugawa nakala ya sera hiyo kwa kila mwajiriwa wake.

Sheria Kiganjani
Learn More
92

Je, mkaguzi anaruhusiwa kufanya uchunguzi eneo la kazi endapo ajali itatokea na kusababisha kifo, ugonjwa au majeraha kwa wafanyakazi?

+

Sheria inamruhusu mkaguzi kufanya uchunguzi juu ya jambo lolote lililotokea eneo la kazi na kusababisha kifo, ugonjwa au majeraha kwa wafanyakazi au mtu yeyote wa karibu.

Sheria Kiganjani
Learn More
93

Je, nani mwenye wajibu wa kuhakikisha kuwa maji safi na salama yanakuwepo kiwandani au mahali pa kazi kwa ajili ya matumizi ya wafanyakazi?

+

Sheria inamtaka mwajiri au mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi kuhakikisha kuwa maji safi na salama na ya kutosha yanapatikana kirahisi kwa ajili ya matumizi ya waajiriwa mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
94

Je, sheria inasemaje kuhusu vyoo kwa waajiriwa wenye ulemavu katika mahali pa kazi?

+

Sheria inamtaka mwajiri kujenga vyoo tofauti kwa ajili ya waajiriwa wenye ulemavu mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
95

Je, Sheria inasemaje kuhusu ukaguzi wa kiwanda kinachotumia umeme?

+

Sheria inasema kuwa kiwanda chochote au mahali pa kazi ambapo umeme hutumika, ukaguzi ufanyike kila mwaka na mkaguzi wa umeme aliyethibitishwa na mmiliki wa kiwanda au mahali pa kazi atapatiwa cheti kinachothibitisha kuwa ukaguzi huo umefanyika

Sheria Kiganjani
Learn More
96

Je, mkaguzi anaruhusiwa kisheria kuchapisha au kuweka hadharani taarifa za kibiashara au za kiutendaji kazi za mwajiri ambazo anaweza kuzipata wakati anatekeleza majukumu yake?

+

Sheria inasema kuwa mkaguzi haruhusiwi kuchapisha au kuweka hadharani taarifa za mwajiri za kibiashara au za kiutendaji kazi anazozipata wakati anapotekeleza majukumu yake. Hata hivyo, kuna mazingira ambapo mkaguzi atatakiwa kuweka hadharani taarifa hizo hasa pale ambapo taarifa hizo zinahitajika kwa ajili ya kuendesha kosa mahakamani au pale ambapo taarifa zinahitajika kwa ajili ya shughuli za kiutendaji chini ya sheria.

Sheria Kiganjani
Learn More
97

Upi ni wajibu wa mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi pale mkaguzi anapofika katika eneo husika kwa lengo la kutekeleza majukumu yake kisheria?

+

Sheria inatoa maelekezo kwa mmiliki wa kiwanda au eneo la kazi au msaidizi wake au mtu yeyote anayehusika kuhakikisha mkaguzi anatekeleza majukumu yake kisheria. Hii inajumuisha kumruhusu kuingia na kufanya ukaguzi na kumpatia nyaraka muhimu atakazozihitaji.

Sheria Kiganjani
Learn More
98

Kila mwaka kuna siku ambayo inatambulika kimataifa kama Siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi. Taja tarehe na mwezi ambapo siku hii huadhimishwa duniani.

+

Siku ya Usalama na Afya duniani huadhimishwa tarehe 28 Aprili ya kila mwaka.

Sheria Kiganjani
Learn More
99

Mfanyakazi ana haki ya kulindwa asipate madhara ya kiafya wakati awapo mahali pa kazi. Haki huendana na wajibu. Je, Sheria ya Usalama na Afya Kazini inampa wajibu wowote mfanyakazi katika suala zima la usalama na afya mahali pa kazi?

+

Ufuatao ni wajibu wa mfanyakazi chini ya Sheria ya Usalama na Afya Kazini; Moja, Kuchukua tahadhari kwa ajili ya usalama na afya yake na mtu mwingine ambaye anaweza kuathirika na vitendo vyake, Mbili, Kushirikiana na mwajiri pale panapowezekana ili kuwezesha mahitaji yaliyowekwa na mwajiri kufikiwa au kuzingatiwa kwa usahihi, Tatu, Kutekeleza amri yoyote ya kisheria yenye dhumuni la kulinda usalama na afya mahali pa kazi, Nne, Kutoa taarifa kwa mwajiri au mwakilishi wa usalama na afya mahali pa kazi juu ya hali yoyote au ajali ambayo inaweza kusababisha madhara kwa afya yake mahali pa kazi.

Sheria Kiganjani
Learn More
100

Nchini Tanzania ni sheria gani inayosimamia usalama wa afya mahali pa kazi?

+

Usalama wa afya mahali pa kazi unasimamiwa na Sheria ya Usalama na Afya na Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake.

Sheria Kiganjani
Learn More
101

Mwajiri yeyote ambaye hajaridhika na maamuzi ya Mkaguzi Mkuu anaweza kuwasilisha rufaa yake kwa Waziri mwenye dhamana ya mambo ya kazi. Je, Waziri baada ya kupokea rufaa hiyo anatakiwa kutoa maamuzi ndani ya muda gani?

+

Waziri mwenye dhamana ya mambo ya kazi baada ya kupokea rufaa anatakiwa kutoa maamuzi ndani ya siku thelathini (30).

Sheria Kiganjani
Learn More

Subscribe to Our News Letter

Subscribe to our newsletter to get the latest news and updates from Sheria Kiganjani

logo

Various Topics

  • The Beginning
  • Topic
  • About
  • Communicate with us
  • Article
  • Landesa

Working Hours

  • Monday - Friday
  • 08:00AM - 5:00PM
  • Saturday
  • 08:00 - 1:00PM

Call us: +255 621 900 555

Email: [email protected]

Visit us

7th Floor, Tanzanite Park Victoria Area POBOX 6622 Dar Es Salaam

Copyright © 2025 All Right Reserved Law in the palm of your hand