Mambo ambayo ni ya msingi ili kufanya muunganiko wa mwanaume na mwanamke uweze kutambuliwa kama Ndoa ni pamoja na haya yafuatayo: a) Hiari : lazima muunganiko utokane na chaguo binafsi la wahusika; bila Udanganyifu, laghai au kurubuniwa kwa aina yoyote b) Kusudio la kudumu: muunganiko wa wanandoa sharti uwe umekusudiwa kuwa wa kudumu, isipokuwa kama litatokea jambo ambalo liko nje ya uwezo wa wanandoa kuzuia kuvunjika kwa muunganiko huo, kama vile kifo cha mmoja wao, talaka, nk. c) Jinsi Tofauti: Ndoa sharti iwe kati ya mtu-mme na mtu-mke; watu wenye maumbile tofauti ya via vya uzazi d) Isihusishe Maharimu: Sheria inazuia ndoa kati yadada na kaka, baba na binti yake, mama na mwanawe, babu au bibi na mjukuu wake, shangazi au mjomba na mpwawe, au baba ama mama mlezi na mtoto aliyemuasili. e) Umri: Kigezo cha umri kimetajwa katika muktadha tofautitofauti, lakini kwa ujumla, wanandoa wanapaswa kuwa na umri wa miaka 18 au zaidi. f) Uwepo wa Ndoa nyingine: Kama mwanamne ana ndoa nyinigne isiyomruhusu kuongeza mke, au kama mwanamke ana mme mwingine basi ndoa hiyo haiwezi kufungwa. g) Kusiwe na Pingamizi: Kabla ya ndoa kufungwa ni lazima tangazo litolewe juu ya kusudio la kufunga ndoa, na ndoa hiyo haitafungwa iwapo kutakuwa na pingamizi halali kutoka kwa mtu mwenye haki ya kufanya hivyo. h) Mfungishaji ndoa awe na mamlaka ya kufanya hivyo: Mfungishaji wa ndoa ni lazima awe na leseni au kibali cha kufungisha ndoa kutoka kwa msajili mkuu wa ndoa. i) Kuwe na mashahidi: Ni lazima wakati wa kufunga ndoa kuwe na mashahidi wasiopungua wawili ambao ni lazima wawe na umri si chini ya miaka 18 na wawe na akili timamu na kuelewa lugha inayotumika katika shughuli hiyo. Pia ni lazima wawepo kwa pamoja kwenye tukio la kufunga ndoa. j) Sharti wafunga ndoa wote wawili wawepo: Wanandoa wote wawili sharti wawepo kwa pamoja wakati wa tukio la kufunga ndoa