Wakati maombi ya kuomba usimamizi au utekelezaji wa mirathi yanaendelea mahakamani, mwombaji anaweza kuiomba mahakama impe usimamizi wa mirathi wa muda. Msimamizi aliyepewa usimamizi wa muda anakuwa na majukumu sawa na msimamizi aliyethibitishwa au kuteuliwa na mahakama ya kukusanya na kutunza mali ya marehemu, isipokuwa hawezi kugawa mali ya marehemu kwa warithi. Lengo la kutoa usimamizi huu wa muda, ni kulinda mali za marehemu zinazoweza kuharibika au kupotea, kuwawezesha kutimiza majukumu ya haraka kama vile matunzo kwa watoto na mjane.